Mzee wa Miaka 75 Aweka Bango la Mke Anayemtaka
Kutoka Dar es salaam.
Katika
hali isiyo ya kawaida mzee mwenye umri wa miaka 75, Athuman Mchambua,
mkazi wa Mtoni kwa Azizi Ally jijini Dar es Salaam amezua gumzo mtaani
baada ya kuamua kutafuta mke kwa kuweka bango barabarani.
Katika
bango aliloliweka katikati ya barabara Mzee Mchambua alianisha sifa
tano za mke anayemtaka pamoja na namba za simu za kuwasiliana naye.
Sifa
hizo ni pamoja na awe mshika dini, uvumilivu wa ndoa, uwezo wa kilimo,
apendo wa mume, watoto na wajukuu pamoja na usafi wa hali ya juu.
Mzee
Mchambua ambaye alizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC
Swahili) hivi karibuni alisema alifanya uamuzi huo baada ya kufiwa na
mke wake aliyezaa naye watoto 11 na kumwacha akiwa hana mtu wa kumsaidia
kutunza familia na kufanya shughuli za shambani.
Katika
mazungumzo na mwandishi wa BBC, alisema tayari wamejitokeza wanawake
wanne waliotaka kuolewa naye lakini hakuna hata mmoja aliyekidhi vigezo
alivyoainisha.
Alisema alilazimika kutumia njia ya tangazo kwa sababu anafiri kwa umri alionao hawezi kumpata mke kwa njia ya kawaida.
Alisema
endapo njia hiyo itashindikana kumpata mke mwenye sifa anazotaka
atalazimika kutumia madalali kumsaidia kumtafuta mke mwenye sifa.
BBC
pia ilizungumza na mmoja wa watoto wa Mzee Mchambua, ambaye alisema
anaona uamuzi wa baba yake ni sawa kwa sababu ameweka sifa za mwanamke
anayemtaka.
Mtoto huyo alisema wapo tayari kumpokea mke mpya wa baba yao na watamheshimu kama mama yao mzazi.