Lekam Hotel

Lekam Hotel
lekam Hotel

Habari na Matukio

Scorpion Akana Hoja 6 . . . . Akiri Hoja 3 Ikiwemo Kupata Mafunzo ya Kareti 

MSHITAKIWA katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, Salum Njwete (34) ‘Scorpion’, amekiri kupata mafunzo ya kareti kutoka chuo cha mafunzo cha Ifakara aliyoyafanya mwaka 1989 hadi 1995.

Aidha, upande wa mashitaka katika kesi hiyo umemuongezea mashitaka ya shambulio kupitia kifungu namba 234 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ambacho kinaruhusu kuongeza au kubadilisha mashitaka.

Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule kwamba kesi hiyo imekuja kwa ajili ya mshitakiwa kusomewa maelezo ya awali ambapo katika maelezo ya zaidi ya saa nane, alikiri kuhusu jina lake, sehemu anayoishi ya Machimbo Yombo na mafunzo hayo.

Hata hivyo, alikana kuhusu jina la Scorpion, mashitaka yake na kwamba hakukamatwa wala kuhojiwa na Polisi kuhusu mashitaka hayo.

Katuga alidai kuwa Septemba 6, mwaka huu, mshitakiwa alikuwa maeneo ya Buguruni Sheli na kwamba Septemba 12, alihojiwa na kukamatwa na polisi maelezo ambayo aliyakana.

“Mashahidi watakaotoa ushahidi katika kesi hii wapo sita ambapo upande wetu wa mashitaka utawasilisha vielelezo viwili ikiwemo Fomu namba tatu ya Polisi (PF3) na ripoti ya daktari kwa ajili ya kuthibitisha mashitaka hayo,’’ alidai Katuga.

Hakimu Haule aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 14 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kusikilizwa. Katika mashitaka yake, mtuhumiwa inadaiwa alitenda kosa hilo Septemba 6, mwaka huu katika maeneo ya Buguruni Sheli, wilaya ya Ilala.

Inadaiwa, Njwete aliiba mkufu rangi ya fedha wenye uzito wa gramu 34 wenye thamani ya Sh 60,000, bangili ya mkononi na fedha taslimu Sh 331,000, vyote vikiwa na thamani ya Sh 476,000 mali ya Said Mrisho.

Inadaiwa kabla na baada ya wizi huo, alimchoma kisu machoni, tumboni na mabegani mlalamikaji ili ajipatie mali hizo

Idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2017 

 

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene amesema kuwa wanafunzi 526,653 kati ya 555,291 waliofaulu mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka huu wamechaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza mwakani katika shule za sekondari za Serikali.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi hiyo ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika awamu ya kwanza ni sawa na asilimia 94.85 ya wanafunzi wote waliofaulu.

Akizungumza na Waandishi wa habari tarehe 28 Novemba 2016 mjini Dodoma Waziri Simbachawene ameeleza kuwa wanafunzi 28,638 wakiwemo wavulana 12,937 na wasichana 15,701 hawakuchaguliwa katika awamu ya kwanza ya uchaguzi.

Aidha Waziri Simbachawene aliitaja mikoa ambayo wanafunzi wake walifaulu lakini hawakuchaguliwa katika awamu ya kwanza kuwa ni pamoja na Dar Es Salaam (18,820), Arusha (4,752), Songwe (1,465), Kigoma (1,208), Manyara (1,141), Lindi (608), Mbeya (406) na Katavi (238).

Kuhusu wanafunzi waliochaguliwa Waziri Simbachawene amesema kuwa, wasichana ni 268,052 sawa na asilimia 94.5 na wavulana ni 258,601 sawa na asilimila 95.2.

Aidha, Waziri wa Nchi amesema kuwa wanafunzi wote wenye ulemavu waliofaulu wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2017.

Kwa mujibu wa Waziri Simbachawene mchanganuo wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za serikali umegawanyika katika makundi manne ambapo kundi la kwanza limehusisha wanafunzi 900 wakiwemo Wavulana 480 na Wasichana 420 ambao wamepelekwa katika shule za Bweni kwa wenye ufaulu mzuri zaidi.

Ameongeza kuwa kundi la pili limehusisha wanafunzi 1005 ikiwa ni Wavulana 915 na Wasichana 90 ambao wamepelekwa katika shule za Bweni mahsusi kusomea Ufundi.

Pia amesema kuwa kundi la tatu limewahusisha Wanafunzi 780 wakijumuishwa Wavulana 430 na Wasichana 350 ambao wamechaguliwa kujiunga na Shule za Bweni Kawaida na kundi la nne limewahusisha wanafunzi 723 wakiwemo wavulana 405 na wasichana 318 wa shule za bweni kwa ajili ya wanafunzi walio na Ulemavu.

Kulingana na takwimu hizo, Waziri Simbachawene amesema kuwa jumla ya wanafunzi 3,407 wamechaguliwa kujiunga na shule za bweni kidato cha kwanza ambapo wavulana ni 2,230 sawa na asilimia 65.4 na wasichana 1,178 sawa na asilimia 34.6, pia watahiniwa wapatao 6,260 sawa na asilimia 0.78 ya waliosajiliwa hawakufanya mtihani.

Aidha Waziri Simbachawene amesema kuwa wanafunzi 523,245 wakiwemo wavulana 256,371 na wasichana 266,874 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za kutwa.

Wakati huo huo Mhe. Simbachawene amesema hatasita kuzichukulia hatua, shule zilizohusika na udanganyifu wa mitihani kwani wanarudisha nyuma maendeleo ya taaluma nchini yanayofanywa na Serikali.

“Serikali imeanza kuwachukulia hatua kwa mujibu wa taratibu wale wote waliohusika na udanganyifu huu� hatua hizo ni pamoja na kuwavua madaraka waliokuwa Waratibu Elimu Kata na Walimu Wakuu, kuwashtaki mahakamani na kupeleka mashauri yao Tume ya utumishi ya Walimu (TSC),” amesema Mheshimiwa Waziri.

Pia ametoa agizo kwa Wakuu wa Mikoa kubainisha sababu za wanafunzi walioingia darasa la kwanza kutomaliza masomo yao kama ilivyotarajiwa.

“Naagiza Wakuu wa Mikoa kubainisha sababu za wanafunzi hao kutomaliza na hatua stahiki za kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaoandikishwa darasa la kwanza wanamaliza mzunguko wa masomo kwa mujibu wa Sera ya Elimu,” amesisitiza Mhe. Simbachawene na kutaka Wakuu wa mikoa kuchukua hatua stahiki zilizoelekezwa.