Lekam Hotel

Lekam Hotel
lekam Hotel

Tuesday, 20 June 2017

Mbinu Tano za Kufanikiwa.

Watu wengi wamekuwa wakitafuta mafanikio maishani lakini tambua kwamba mafanikio ya kweli yatapatikana...


Watu wengi wamekuwa wakitafuta mafanikio maishani lakini tambua kwamba mafanikio ya kweli yatapatikana tu ukiwa na bidii, ustahimilivu, nidhamu pamoja na shauku kubwa ya kupata mafanikio. Zifuatazo ni mbinu tano muhimu zitakazo kusaidia kuwa mstahimilivu katika harakati za kutafuta maendeleo na mafanikio.

1. Fahamu matakwa yako.

Ninachomaanisha hapa ni kujua nini unataka, ukijua unachotaka utakuwa na msimamo wa kutaka kufikia malengo yako. Kama bado hujui nini unataka basi nakushauri ufanye hivi, chukua kalamu na karatasi kisha jiulize Unataka kufanikiwa kitu gani? Hapa ni muhimu wakati ukijiuliza unataka kufanikiwa nini basi ujitahidi kutofikiria mawazo hasi au mawazo mabaya ya kujiona kama utashindwa kufanikiwa. Jiamini, ondoa hofu au wasiwasi wowote utakaokuwa nao na orodhesha mambo yote unayotaka kufanikiwa katika karatasi yako na kisha anza kupanga mipango kwa kujiwekea malengo na kutekeleza moja baada ya jingine.

2. Nini kinakupa motisha au hamasa ya kutaka kufanikiwa.

Motisha ni chachu ya ustahimilivu kwani hukufanya kuendelea kushikamana na mipango yako mpaka mwisho licha ya kuwa na vipingamizi vingi katika njia yako ya mafanikio. Malengo mengine Ni ya muda mrefu hivyo yanakuhitaji uwe mvumilivu ili ufanikiwe, kama utakosa ustahimilivu wa kungojea matokeo unaweza kujikuta unakata tamaa mapema kabla ya kufikia malengo. Motisha ni kitu pekee kinachokusaidia kukusukuma uendelee kutaka kufanikiwa hivyo ni heri kila malengo unayojiwekea yawe ni yenye kukupa kiu ya kutaka kufanikiwa kwakuwa unapenda hayo unayohangaikia.

3. Jenga nidhamu na tabia ya kushikamana na kitu ulichoanza mpaka ufikie mwisho wake.
Ni vizuri kuwa na malengo ila malengo hayo kama hutakuwa na nidhamu ya ustahimilivu yatakuwa ni bure kwako kwani hutafanikiwa katika jambo lolote.‘’Discipline is the bridge between goals and accomplishment.’’ –Jim Rohn. Katika kuyaendea malengo yako utakutana na changamoto au vikwazo vingi sana, ni nidhamu ya ustahimilivu pekee ndio itakayo kufanya uendelee kudumu katika kufuata malengo yako ama sivyo unaweza kutetereka na kujikuta upo mbali na malengo uliyojiwekea na kushindwa kufanikiwa.

4. Tathmini hatua utakazopitia Ili kufikia malengo yako.


Licha ya kutambua nini unataka, kujua pia utafanyaje ili kufikia malengo yako ni jambo la msingi sana. Maana Kama hutojua utaanzaje au utafanyaje ili ufikie malengo yako ni rahisi kupoteza dira ya wapi unaelekea na mwishowe kutofanikiwa. Pata picha halisi ya nini utafanya Na wapi utapitia ili ufanikiwe lasiivyo utajikuta umekwama mahali na kushindwa kuyafikia malengo yako.

5. Jenga fikra chanya kwa kuamini unayotaka kufanya yanawezekana.

Safari ya mafanikio sio rahisi kama watu wengi wanavyofikiria, kila aliyefanikiwa ana hadithi yake ya kusimulia juu ya changamoto alizokumbana nazo katika jitihada za kutafuta mafanikio. Kama hutokuwa na imani thabiti ya kile unachofanya ni vigumu kuwa na matumaini ya hicho unachokifanya kuwa kinawezekana na unaweza kufanikiwa. Hofu, wasiwasi na mashaka ni adui wa maendeleo epuka hivi vitu kwa kuamini utafanikiwa.

Tunakutakia safari njema ya mafanikio uhuru na maendeleo yako,Nasi tuko pamoja na Mungu Akubariki karibu tena TIFC